Israel yashambulia kambi za kijeshi za Syria kufuatia shambulio la milima ya Golan
Ndege za kijeshi za Israel zimeshambulia kambi za kijeshi za Syria siku ya Jumatatu, Jeshi la Israel lilithibitisha katika taarifa isio ya kawaida.
Vyombo vya habari vya Syria vilikiri mashambulio hayo, vikiripoti uharibifu katika kambi moja iliopo kandokando ya mji mkuu wa Damascus.
Jeshi la Israel IDF lilisema kwamba lilikuwa likijibu jaribio la shambulio la makombora.
Jeshi hilo limesema kwamba awali lilikuwa limewaua watu wanne waliokuwa wakiweka vilipuzi katika ardhi inayokaliwa na Israel katika milima ya Golan jioni siku ya Jumapili.
Kanda za video zilionesha kundi hilo likijipata katika milipuko.
Msemaji wa Jeshi Luteni kanali Jonathan Conricus alisema kwamba ilikuwa mapema mno kusema iwapo wanaume hao walitoka katika kundi fulani, lakini Israel ikalaumu serikali ya Syria.
''Shambulio la siku ya Jumatatu lililenga vituo vya uchunguzi, mifumo ya kijasusi, makombora ya kudengua ndege na mifumo ya usimamizi wa kijeshi katika kambi za majeshi ya Syria katika mji wa Qunaitra'', lilisema jeshi la Israel.
Jeshi la Israel linalaumu serikali ya Syria kwa vitendo vinavyotokea katika ardhi ya Syria, na litaendelea kufanya operesheni zake kwa nguvu dhidi ya ukiukaji wowote dhidi ya Uhuru wa Israel, ilisema taarifa hiyo.
Chombo cha habari cha Syria Sana kiliripoti kwamba jeshi la Syria lilishambulia maeneo ya adui karibu na mji mkuu wa Damascus.
Wakati huohuo shirika la haki za kibinadamu Oservatory for Human Rights limesema kwamba mashambulia ya alfajiri yaliofanyika katika mji wa Boukamal, karibu na mpaka wa Iraq kaskazini mashariki yamewaua watu 15.
Hali ya wasiwasi imeanza kuongezeka kati ya mahasimu Israel na Syria, hususan katika eneo la kaskazini lenye wanajeshi wa Israel , tangu shambulio la Israel kumuua mpiganaji mmoja wa kundi la Hezbollah nchini Syria wiki mbili zilizopita.
Israel ilitarajia kwamba kundi hilo la Lebanon linaloungwa mkono na Iran litalipiza kisasi.
0 Comments